Kocha Msaidizi wa Simba Selemani Matola amesema wamekiandaa kikosi kuhakikisha wanaondoka na ushindi katika mchezo wa dabi dhidi ya Yanga ambao utapigwa Jumamosi, May 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika kikao cha mechi kilichoandaliwa na TFF mbele ya Wanahabari, Matola amesema wanaingia katika mchezo huo huku kikosi kikosi chao kikiwa na utulivu, wachezaji wote wakiwa timamu
Aidha amesema msimu huu wamecheza mechi kubwa katika ligi ya mabingwa hivyo ana imani kuwa watakuwa na nafasi ya kushinda
"Wachezaji wote wako tayari kwa mchezo, hatuna majeruhi hili ni jambo linalotupa matumaini kuwa tutafanya vizuri"
"Kwa bahati nzuri tumecheza mechi kubwa katika michuano ya ligi ya mabingwa hivyo wachezaji wetu wamepata uzoefu mkubwa ambao utawasaidia katika mchezo wa kesho"
"Kiuchezaji tutakuwa tofauti kulinganisha na michezo tuliocheza na Yanga nyuma, tuna kocha mpya ambaye amekuja na mbinu tofauti lakini pia tulipitia michezo yetu ya nyuma kuangalia wapi tulikosea na wapi tulipatia tuweze kuendeleza"
"Nawaambia mashabiki wa Simba waje kwa wingi uwanjani, tutacheza vile ambavyo tumezoea, hakuna kitakachobadilika kwa kuwa ni mchezo wa dabi. Watapata burudani na bila shaka tutawapa furaha baada ya dakika 90," alisema Matola