Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara, amesema kwa ubora wa kikosi cha Simba, wanahitaji wachezaji kujitoa kwa angalau asilimia 75% kupata ushindi dhidi ya Yanga
Manara amesema kwa mujibu wa takwimu, kizazi cha Simba ya sasa ndio kizazi bora kilichowahi kutokea hivyo hadhani mchezo dhidi ya Yanga utawasumbua siku ya Jumamosi
"Huwezi kunitajia timu bora ya Simba iliyowahi kutokea kuizidi hii. Hii Ni timu bora zaidi kwenye kila kitu, tukizungumzia kwa takwimu, rekodi , Style, Playing System"
"Kama wachezaji wa Simba wakifikia 75% ya ubora wao Siku ya Jumamosi , Yanga watakufa bao mbili kwenda mbele . Kuifunga Yanga itakua kama kufunga Ramadhan," alitamba Manara katika mahojiano na Wasafi FM
Manara amesema Simba imejiwekea malengo ya kuvunja rekodi zote zilizowekwa miaka ya nyuma
"Simba ilikuwa timu ya mwisho kuchukua ubingwa wa ligi kwa misimu mitano mfululizo. Tangu mwaka 1980, hakuna timu iliyowahi kuchukua ubingwa wa ligi kwa zaidi ya misimu mitatu hivyo kizazi hiki cha Simba kinaenda kuvunja rekodi hiyo kwa kuchukua ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo"
"Mwaka 1974 Simba ilifika nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wakati huo timu ikiwa na akina Kibaden (Abdallah) lakini walicheza takribani michezo mitatu kufika hatua hiyo. Kikosi chetu kimedhamiria kufika nusu fainali, na tukifanya hivyo tutavunja rekodi iliyowekwa na kina Kibaden kwa kulinganisha ushindani wa wakati ule na sasa," aliongeza Manara