Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Kim Poulsen jana alitangaza majina ya wachezaji 43 alioita kuunda kikosi chake kitakoweka kambi jijini Dar es salaam kabla ya kuelekea nchini Kenya ambapo watacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Harambee Stars
Kikosi hicho kinatarajiwa kucheza mechi mbili za kufuzu fainali za Afcon 2022 dhidi ya Guinea ya Ikweta na Libya
Miongoni mwa wachezaji walioitwa, 10 wanatoka klabu ya Simba
Hata hivyo Poulsen alitoa ufafanuzi kuwa wachezaji wa Simba wao wataingia kambini March 18 baada ya mchezo wao wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Merreikh ambao utapigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam
Ikumbukwe Simba wataanzia nchini Sudan kuwavaa Al Merreikh March 05 katika mchezo wa raundi ya tatu na ule utakaopigwa jijini Dar es salaam utakuwa wa raundi ya nne
Simba inahitaji alama zote sita kutoka kwa Al Merreikh ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali mapema
Wachezaji wa Simba walioitwa Stars ni Aidhi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, John Bocco na Jonas Mkude