Mabingwa wa nchi Simba leo wanashuka pale uwanja wa Benjamin Mkapa mishale ya saa 11 jioni kuikabili Al Hilal katika mchezo wa kukata na shoka michuano ya Simba Super Cup
Mashabiki wa Simba watakuwa na nafasi ya kuona kikosi chao kilichoboreshwa kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa hatua ya makundi ambayo itaanza mwezi ujao
Huu ni mchezo wa kirafiki unaowakutanisha mabingwa wa Tanzania na Sudan ukiwa ni maandalizi kwa timu zote kwa kampeni ya michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu
Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amesema mechi hizi za Super Cup zitamsaidia kuwafahamu vizuri wachezaji wake na kumpa mwanga wa nini anapaswa kufanya
Lakini jambo moja muhimu, Gomes amesema amevutiwa na uwezo ulioonyeshwa na wachezaji wake katika siku mbili alizofanya nao mazoezi hivyo anaamini watashinda mashindano haya
Baada ya mchezo wa leo, mchezo utakaofuata ni kati ya Al Hilal dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa keshokutwa Ijumaa na Jumapili Simba itakamilisha michuano hii kwa kuumana na TP Mazembe
Hii ni wiki ya burudani kwa mashabiki wa Simba na wapenda soka wote nchini