Wakati klabu ya Simba ikikimbilia TFF kulalamika kuwa Yanga imeanza mazungumzo na kiungo wao Clatous Chama ambaye ana mkataba na timu hiyo, wakitumia kauli ya Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela aliyoitoa juzi wakati akihojiwa na redio moja maarufu nchini, kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael amesema hayo ni maigizo ya usajili kwani Chama sio miongoni mwa wachezaji aliopendekeza wasajiliwe
Eymael ambaye bado amekwama Ubelgiji kutokana na changamoto ya usafiri iliyosababishwa na janga la corona, amesema hajawahi kumfikiria kiungo huyo wa Simba hivyo anadhani kinachoendelea sasa ni tetesi za usajili ambazo ni kawaida kutokea na kupotea
"Sina jina la Chama kwenye orodha ya wachezaji ninaowataka, nafikiri hayo ni maigizo ya usajili tu lakini ki ukweli hatukuwahi kuwa na mpango na mchezaji huyo," alisema
Jana Mwakalebela aliomba radhi kwa kauli aliyoitoa juzi akieleza kuwa alikuwa akifanya masihara na hakuna mpango wowote wa Yanga kumsajili Chama
Hata hivyo Simba imepeleka malalamiko TFF ambapo Shirikisho hilo limethibitisha kupokea malalamiko hayo na kuyafikisha kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji
Jambo hilo huenda likamalizwa 'kiungwana' kwa kuwa tayari Mwakalebela amejitokeza hadharani kuomba radhi