Mlinda lango wa Simba Aishi Manula amesema baada ya kukamilisha mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu Fc wakifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 4-0, sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Platinum Fc ambao utapigwa wiki ijayo katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza baada ya mchezo huo ambao Simba ilifunga mwaka 2020 kwa ushindi wa kibabe, Manula amesema mawazo yao sasa ni kuelekea mchezo dhidi ya Platinum wakiwa na malengo ya kutinga makundi
Mlinda lango namba moja wa timu ya Taifa, amesema wanafahamu wataingia katika mchezo huo wakiwa nyuma kwa bao moja, lakini hilo haliwapi wasiwasi
"Wachezaji wote tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mchezo dhidi ya Platinum. tunajua mchezo wa kwanza tulifungwa ugenini na sisi tunawasubiri hapa nyumbani. Wanasimba waje kwa wingi uwanjani wasiwe na hofu, tumedhamiria kuwapa furaha," alisema Manula
Kuelekea mchezo huo, kaulimbiu wanayotumia Wanamsimbazi ni War in Dar (WIDA), ikimaanisha vyovyote itakavyokuwa lazima Platinum Fc 'wapasuke' pale kwa Mkapa