Mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Afcon 2021 kati ya Tanzania dhidi ya Tunisia, umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1
Haukuwa mchezo mwepesi kwa Stars ambayo lango lake lilikuwa katika kashikashi kwa muda mwingi, vijana wa Tunisia wakiwa bora zaidi
Tunisia walitangulia kufunga bao kupitia kwa Khoul kwenye dakika 11 baada ya kufanya shambulizi kali langoni kwa Stars
Kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri sana kwa vijana wa Stars ambao walionekana kushindwa kwendana na kasi ya Tunisia
Hata hivyo Stars walirejea wakiwa imara zaidi kwenye kipindi cha pili na walihitaji dakika mbili tu kusawazisha bao kupitia kwa kiungo Feisal Salum
Feisal alifunga bao maridhawa kwa shuti kali nje ya 18 akitengewa pasi murua na nahodha John Bocco
Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha Stars ambayo iliendelea kupeleka mashambulizi langoni kwa Tunisia lakini hawakufanikiwa kuutumbukiza mpira wavuni
Katika dakika 20 za mwisho Tunisia wakazinduka tena wakilisakama lango la Stars lakini umahiri wa mlinda lango Aishi Manula uliiweka salama Stars
Ditram Nchimbi angeweza kuifungia Stars bao dakika za majeruhi baada ya kichwa alichopiga kutoka sentimita chache langoni kwa Tunisia
Ni matokeo ambao alama moja kwa Stars inaweza kuwa na maana kwani haukuwa mchezo mwepesi
Stars imefikisha alama nne, itahitaji kushinda mechi zake mbili zilizobaki mwakani kuweza kufuzu kwa fainali za Afcon zitakazopigwa Cameroon mwakani