Mwaka 1993 utaendelea kubaki katika kumbukumbu za mashabiki wa klabu ya Simba na Watanzania kwa ujumla kwani ni mwaka ambao Simba ilikaribia kutwaa ubingwa wa kombe la Washindi (CAF) jijini Dar es salaam
Simba ilifanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo dhidi ya Stella Abidjan ya kule nchini Ivory Coast
Mchezo wa kwanza ulipigwa ugenini Ivory Coast na Simba iliyokuwa ikinolewa na kocha mzawa Abdallah Kibaden 'King' iliweza kupata matokeo ya suluhu ya bila kufungana
Lakini kwa bahati mbaya, Simba ilishindwa kutwaa taji hilo katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Jumamosi, Novemba 26, 1993 baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0
Simba kabla ya kucheza na Stella Abidjan, ilianza michuano hiyo kwa kuitoa Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka suluhu mjini Mwanza katika raundi ya kwanza.
Katika raundi ya pili, Simba iliitoa Manzini Wanderers ya Swaziland kwa jumla ya mabao 2-0. Katika mchezo wa robo fainali ikainyuka klabu ya Al Harrach ya Algeria kwa mabao 3-2 na katika mchezo wa nusu fainali iliiondosha Atletico Sports Aviacao ya Angola kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba baada ya kushinda katika mchezo wa nusu fainali ndio hapo sasa ilipocheza na Stella Abidjan na kushuhudia Kombe la CAF likiondoka katika ardhi ya Tanzania na kupanda ndege kuelekea Ivory Coast.
Mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, walikuwa na kila dalili ya matumaini ya kutwaa taji hilo kabla ya mechi kuchezwa.
Baada ya matokeo hayo baadhi ya wachezaji waliingia matatani wakituhumiwa kuuza mechi, lakini hakuna uthibitisho wowote kutokana na tuhuma hizi ambazo zilitolewa na wengi hasa baada ya kupoteza mchezo huo muhimu nyumbani hasa ikizingatiwa timu ilifanya vizuri ugenini
Kikosi kilichoiwakilisha Simba wakati huo ni kipa Mohamed Mwameja, Kasongo Athumani, Rashid Abdallah, Godwin Aswile, George Masatu, Iddi Seleiman, George Lucas, Hussein Marsha, Malota Soma/Michael Paul, Edward Chumila (marehemu)/Thomas Kipese na Damian Mrisho ‘Kimti’ (marehemu)