Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema wanawakaribisha mashabiki wa Yanga kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kushuhudia kandanda bora kutoka kwa machampioni wa nchi
Jioni ya leo Simba itakuwa mgeni wa JKT Tanzania katika mchezo utakaopigwa dimba la Jamhuri
Manara amesema mashabiki wa Simba ni waungwana, hawana mambo ya hovyohovyo ya kupigana
Amewahakikishia mashabiki hao wa Yanga kuwa hamna ambaye atapigwa wala kufinywa
Manara aliyazungumza hayo jana usiku kwenye hafla maalum ya kibingwa iliyofanyika mkoani Dodoma
Aidha Manala amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani kama ilivyo kawaida yao, kuwaunga mkono wachezaji wao kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu
"Mashabiki wa Yanga si mpo mmehudhuria hafla hii?, na kesho njooni uwanjani mshuhudia kandanda safi. Sisi hatupigani, nawahakikishia hakuna mtu atakayepigwa wala kufinywa," alisema Manara
Juzi TFF ilichukua hatua ya kuwafungia mwaka mmoja mashabiki wa Yanga waliobainika kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba waliokwenda mkoani Morogoro kushuhudia mchezo kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga wiki iliyopita