Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara, amemuomba radhi Elias Mwanjala Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kufuatia matamshi aliyoyatoa wakati wa sakata la Bernard Morrison
Juzi kabla ya kutolewa kwa hukumu iliyompa ushindi Morrison dhidi ya klabu ya Yanga, Manara alimtuhumu Mwanjala kuwa alikuwa na mpango wa kutaka kuibeba klabu ya Yanga ambayo yeye ni Mwanachama
Hata hivyo Mwanjala alieleza kutofurahishwa na kauli hiyo aliyoiita ya vitisho kwake kwani Maamuzi katika Kamati hakuwa akifanya yeye peke yake
"Nimewasiliana na Mwanjala, nimemuomba radhi yeye na mtu mwingine yeyote ambaye alikwazika na yale niliyoyazungumza juzi. Lazima ifahamike, mazingira yaliyokuwa yakijadiliwa katika makundi mitandaoni na hata kauli za baadhi ya Wanahabari yalionyesha dalili za waziwazi kuwa yangetolewa maamuzi ya upendeleo"
"Mimi ni mtu muungwana, nimelelewa katika maadili ya kiungwana sana hivyo inapotokea nimemkwaza mtu yoyote ni wajibu wangu kumuomba radhi," alisema Manara