Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano ndani ya mabingwa wa nchi, Haji Manara amewataka mashabiki wa Simba wasitishwe na tetesi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchezaji wao kiungo Mzambia Clatous Chama 'Mwamba wa Lusaka' kwani bado ni mali ya Simba mpaka Julai 21 2021
Manara amesisitiza kuwa Chama bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba na kama Yanga wanamtaka kweli basi wanahitaji kuwasilisha sio chini ya dola laki tatu kuweza kumsajili
"Wala msitishwe na tetesi zinazoenezwa kuhusu kiungo wetu Chama, ana mkataba na Simba mpaka July 2021 hata hao Yanga wanafahamu hivyo. Kama wanamtaka waje wanunue mkataba wake kwa dola 300,000 (zaidi ya Milioni 697.5 za Kitanzania)," alisema Manara
Kumekuwa na tetesi nyingi kumuhusu Chama tangu jana hasa baada ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba Senzo Mazingisa kujiunga na Yanga
Uongozi wa Simba umewataka mashabiki kutoyumbishwa na yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohammed Dewji 'Mo' alisema Simba iko imara na itaendelea kuwa imara na kuondoka kwa Senzo haliwezi kuwa pigo kwao
Simba inatarajiwa kumtangaza Kaimu Mtendaji Mkuu wakati wowote ili kuziba nafasi iliyoachwa na Senzo wakati mchakato wa kumtafuta Mtendaji mwingine ukiendelea