Kwa sasa tetesi kubwa za usajili zinazoihusu klabu ya Simba ni dili la nyota wa Orlando Pirates Justine Shonga ambaye mabingwa hao wa nchi wamekuwa wakitajwa kumuwania
Shonga raia wa Zambia mwenye umri wa miaka 23, anazungumzwa sana hata huko kwao Zambia kuwa yuko njiani kuelekea Msimbazi
Inaelezwa nyota huyo hana furaha kwenye kikosi cha Pirates baada ya kupoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza baada ya Pirates kumsajili Ghabadinho Mhango raia wa Malawi
Hivi karibuni Shonga aliuambia mtandao wa Kick-off wa Afrika Kusini kuwa hatakuwa na pingamizi kujiunga na Simba kama mabingwa hao wa Tanzania Bara watamalizana na Pirates
Hata hivyo Shonga alisema hakukuwa na mazungumzo yaliyokuwa yameanza
Dau la usajili ambalo Pirates wamemuwekea mshambuliaji huyo ni dola 550,000 ambazo ni zaidi ya Bil 1.2 za Kitanzania
Nyota huyo pia ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi cha Pirates akiramba karibu Tsh Milioni 38 kwa mwezi
Gharama za kumpata mchezaji huyo zinaonekana kuwa juu hata hivyo lolote linaweza kutokea kwani kulingana na Mtendaji Mkuu wa Simba Senzo Mazingisa, wamejipanga na hata ikibidi kutumia gharama kuwapata wachezaji waliopendekezwa na Mwalimu ili kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi imara kitakachofanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
Kama usajili wake utafanikiwa, ataungana na nduguye Mzambia Clatous Chama ambaye yeye ameshajijengea ufalme Msimbazi