Michael Sarpong ni mshambuliaji hatari wa Rayon Sports ambaye jina lake linatajwa sana kutakiwa na Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo ambalo utafunguliwa mwezi ujao
Sarpong mshambuliaji wa Kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 23 ni miongoni mwa wachezaji walioorodheshwa kufuatiliwa kwa ukaribu na Yanga ambayo imedhamiria kuimarisha kikosi chake wakati wa dirisha dogo
Msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Rwanda akitupia kambani mabao 16 na kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa
Alifunga jumla ya mabao 22 kwenye mashindano yote
Pamoja na Yanga kufanya usajili mkubwa dirisha lililopita, usajili huo haujamaliza changamoto katika baadhi ya nafasi
Baadhi ya nyota wapya wameshindwa kufikia matarajio
Inaelezwa wakati wa dirisha dogo baadhi ya wachezaji wa kigeni watauzwa au kutolewa kwa mkopo ili kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kusajiliwa
Safu ya ushambuliaji ni moja ya eneo ambalo linahitaji kuongezwa nguvu, Sarpong akitajwa kuchukua nafasi ya mmoja wa washambuliaji waliopo
Msimu huu Yanga imedhamiria kurejesha ubingwa wa ligi kuu walioupoteza kwa watani zao Simba kwa misimu miwili sasa
Lakini mpaka sasa Yanga bado haionekani kuwa na ubavu wa kushindana na wapinzani wake katika mbio za ubingwa Simba na Azam Fc ambazo zimeanza ligi kwa kushinda mechi zao zote
Nyota wengine wanaotajwa kuelekea Jangwani wakati wa dirisha dogo ni pamoja kiungo Haruna Niyonzima, beki wa kushoto Erick Rutanga, mshambuliaji wa UD Songo Luis Miquissone na winga wa Tanzania Prisons Ismail Kada