Nahodha Msaidizi wa Simba Mohammed Hussein 'Tshabalala' amesema jambo analolifikiria zaidi ni kuiona klabu yake ikicheza fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Tshabalala alikuwa sehemu ya kikosi kilichofanya mambo makubwa mwaka juzi baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo wakitolewa na TP Mazembe kwa kufungwa mabao 4-1 baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam
Tshabalala amesema baada ya mafanikio waliyopata mwaka juzi, kila mchezaji ana kiu ya kuona wanafika fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu
"Kila mchezaji hapa kwetu anahitaji kuona mafanikio, kubwa ni kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa, hali hiyo inatulazimu tupambane kuhakikisha tunachukuwa ubingwa na kujipanga kwa michuano hiyo ya kimataifa," amesema Tshabalala.
Beki huyo mahiri kwa upande wa kushoto kwa Tanzania sasa, amesema anashirikiana na wenzake katika kufikia malengo yao hayo akiamini kujituma kwao kutawezesha kuwapa mashabiki kile wanachokitarajia.
"Kwa kipindi hichi cha mlipuko wa virusi vya corona, tupo makini sana kwa sasa, nafanya mazoezi binafsi kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi huku nikijilinda na kuzingatia yale yaliyokatazwa na wizara ya afya"