Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere anatisha katika kupachika mabao kwani mpaka sasa amezifunika baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi kuu
Kagere ndiye kinara wa ufungaji mabao katika Ligi Kuu Bara, ambapo baada ya kufunga bao moja juzi dhidi ya Namungo FC, anakuwa amefikisha mabao 12, idadi ambayo imeshindwa kufikiwa na klabu za Ndanda Fc na Singida United
Ndanda wamefunga mabao sita pekee katika michezo 16, waliyocheza ikiwa ni nusu ya yale aliyofunga Kagere, huku wakikusanya pointi tisa, wakifungwa mechi tisa, sare sita na kushinda mchezo mmoja, wakiwa wanaburuza mkia kwenye msimamo
Wakati kwa upande wa Singida United, wenyewe wamefunga mabao nane katika michezo 17 waliyocheza, wakivuna pointi 10, baada ya kushinda michezo miwili, sare katika michezo minne na kupoteza mechi 11, wakiwa wanashika nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi hiyo.
Aidha Kagere anahitaji kufunga mabao matatu tu ili kuweza kufikia idadi ya mabao 15 ambayo yamefungwa na Yanga mpaka sasa
Mnyarwanda huyo anafukuzia kiatu cha pili cha ufungaji bora baada ya msimu uliopita kuondoka na kiatu hicho baada ya kufunga mabao 23