Baada ya kambi ya takribani wiki tatu mkoani Morogoro, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam kesho Ijumaa August 02 kukamilisha maandalizi ya mwisho kabla ya kuikabili Kariobangi Sharks August 04 siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi
Yanga ilikuwa ikijifua mkoani Morogoro chini ya kocha Msaidizi kabla ya kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera kurejea na kuendelea na majukumu yake siku ya Jumatatu
Mcongomani huyo amesema kwa kiasi kikubwa kikosi chake kimeiva, 'fitnes' ya wachezaji iko vizuri isipokuwa wachezaji wachache ambao walichelewa kuripoti kambini
Hata hivyo amesema hana wasiwasi na vijana wake, watakuwa tayari kwa mchezo wa Jumapili na baadae mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
"Nimewaangalia wachezaji kwenye michezo miwili ya kirafiki tuliyocheza, nimeridhishwa na utayari wao isipokuwa wachache ambao walichelewa kuingia kambini," amesema
"Lakini baada ya siku chache naamini nao watakuwa sawa na wenzao"
"Tuna timu nzuri, msimu ujao tutakuwa vizuri sana kuliko msimu uliopita"
Baada ya mchezo wa August 04 dhidi ya Kariobangi Sharks, Yanga itakuwa na takribani wiki moja kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuikabili Rollers