Mwanzilishi wa Simba Day na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ametoa neno kuelekea tamasha hilo, litakalofanyika keshokutwa Jumanne, kwamba wanachama wajitokeze kwa wingi kuwatakia baraka wachezaji wao
Simba Day ilianzishwa chini ya Dalali mwaka 2009 na imekuwa ikiendelezwa na kila kiongozi anayeingia madarakani
Dalali amesema wanachama wakijitokeza kwa wingi itasaidia kila mmoja kwa imani yake kukibariki kikosi chao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 23 mwaka huu na kwamba utakuwa na ushindani mkubwa.
"Lengo kuu la Simba Day, nikutambulisha silaha zetu za kufanya kazi kwa msimu mpya ili kujuana na wanachama baada ya kuwasikia kwenye usajili, hapo watapata baraka zote kwa Wanasimba.
"Kukusanya pesa za kujenga uwanja, kutambulisha jezi za wachezaji, kurudisha shukrani kwa jamii kwa maana ya wale ambao wanatuunga mkono katika kazi zetu kufanya kitu kwa ajili yao," amesema.
Dalali amesema kuna haja kwa wanachama wa Simba kutoka mikoa yote ya Tanzania kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanafanya kitu kwa ajili ya siku hiyo, kuwa ni muhimu kwa ajili ya kuandaa mikakati itakayowafanya watetee ubingwa.
"Kila klabu ina utaratibu wake, Simba tuna siku ya Simba Day ambayo wiki nzima tunakuwa tunafanya vitu mbalimbali vya kijamii ambavyo sasa tutahitimisha kwa pamoja na kuwatakia kila la heli wachezaji wetu kutimiza majukumu ya klabu"