Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kikosi chake kimetua mkoani Mwanza kusaka alama tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi
Akizungumza baada ya kuwasili jijini Mwanza, Zahera amesema wamefanya maandalizi ya kutosha tangu waliporejea kutoka mkoani Lindi
"Tumefanya mazoezi siku mbili Dar es salaam na pia tutafanya mazoezi siku mbili hapa Mwanza," amesema Zahera
"Hilo litatusaidia kwa wachezaji wetu kuwa tayari kwa mchezo.
"Tulipoenda kucheza na Namungo hatukupata muda wa kufanya mazoezi, tulitoka hapa Mwanza kucheza na Mbao FC"
"Ndio maana katika mchezo ule kuna wakati wachezaji wetu walikuwa wanachoka lakini mchezo dhidi ya Alliance Fc utakuwa tofauti"
Zahera amesema timu yake inacheza kila mchezo ikiwa na lengo la kupata alama tatu hivyo mchezo dhidi ya Alliance hautakuwa na tofauti
Katika hatua nyingine Zahera ameunga mkono mapendekezo ya uwanja wa CCM Kirumba kutumiwa na Yanga kama uwanja wake wa nyumbani wakati uwanja wa Taifa utakapokuwa umefungwa
Zahera amesema uwanja wa CCM Kirumba ni mzuri na sio mbali kutoka jijini Dar es salaam kwa usafiri wa Ndege
"Uwanja wa CCM Kirumba ni mzuri, pia ni mwendo wa saa moja tu kwa ndege kutoka Dar es salaam hivyo utakuwa ni uamuzi mzuri kwa viongozi wa Yanga kama wakiamua kutumia uwanja huu," amesema
Uwanja wa Taifa utafungwa rasmi baada ya mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kati ya Tanzania na Uganda utakaopigwa March 24