Baada ya kukaa muda mrefu bila kuwa na mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatarajia kutangaza mdhamini wa ligi hiyo msimu ujao
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza mkutano na Waziri Mwakyembe Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, alisema wanatarajia kumtangaza mdhamini huyo kabla ya Agosti 15 mwaka huu.
"Mwezi ujao tunatarajia kumtangaza mdhamini wa Ligi Kuu msimu ujao mazungumzo yakikamilika tutamtaja mdhamini tuliyempata," alisema Karia.
Alisema hawakurupuki kuchukua mdhamini bali wanachukua mdhamini anayeendana na hadhi ya ligi yetu.
Karia aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Wachezaji wa Ndani (CHAN) kati ya Taifa Stars na Harambee Stars ya Kenya Jumapili ya Wiki hii jijini Dar es Salaam.
"Mchezo wa Jumapili ni wa kulipa kisasi naamini vijana watafanya vizuri tunaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yetu tusonge mbele," alisema.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura alisema msimu ujao hakutakuwa na viporo vingi kama ilivyokuwa msimu uliopita.
"Nakiri msimu ujao hautakuwa na upungufu wa viwanja na hakutakuwa na viporo vingi kama msimu uliopita, alisema Wambura.