Leo Simba imenasa moja ya majembe ya kazi baada ya kumsajili aliyekuwa kiungo wa Al Hilal Sharaf El Shiboub aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja mbele ya Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Salim Abdallah 'Tray Again'
Sharaf ni kiraka anayeweza kucheza nafasi zote za kiungo pamoja na nafasi ya ulinzi wa kati
Ni mchezaji makini, mtulivu awapo uwanjani na anasifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi
Alianza kuichezea timu ya Taifa ya Sudani akiwa na umri wa miaka 17 tu na bado anaendelea sasa akiwa na miaka 24
Ameibuka kuwa kiungo bora wa ligi kuu ya Sudani kwa misimu miwili mfululizo ambapo pia ameiongoza Al Hilal kutwaa mataji matatu mfululizo ya ligi kuu ya Sudani
Uwezo wake wa kumiliki mpira unaweza kumfananisha na fundi Clatous Chama au Haruna Niyonzima, kwani mpira unapokuwa mguuni kwake 'unatii' kile anachotaka
Ni usajili ambao umezingatia zaidi michuano ya ligi ya mabingwa, suala la kupewa mkataba wa mwaka mmoja ni makubaliano kati ya mchezaji na timu hasa kwa kuangalia gharama za mkataba wenyewe
Lakini kwa wasifu wake hakuna shaka mashabiki wa Simba wasubiri burudani tu kwani wameletewa fundi mwingine wa mpira