Kiungo fundi Thabani Scara Kamusoko muasisi wa 'kampa kampatena' ametoa ufafanuzi wa ujumbe alioweka katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram baada ya kuibuka sintofahamu miongoni mwa mashabiki wa Yanga juu ya hatma yake klabuni hapo.
Jana Kamusoko aliandika ujumbe wa kuwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa upendo na ushirikiano waliompa tangu alipotua Yanga misimu minne iliyopita.
Siku chache zilizopita pia aliandika ujumbe akiwauliza mashabiki iwapo aendelee kubaki Tanzania au aondoke.
Mkataba wa mkongwe huyo unamalizika mwezi wa sita, wengi wanaamini fundi huyo huenda akaondoka Yanga mkataba wake utakapomalizika.
"Mimi bado nipo Yanga, toka nimefika hapa nimepewa upendo ambao ni vigumu kuelezea nikaona nami napaswa kusema ahsante na kuonesha kuwa nakubali na kuheshimu thamani nnayopewa," amesema
"Sio kama naondoka Yanga, hapana mimi nipo nipo sana. Naomba Wana Yanga wasielewe tofauti maana wengine wanaweza wakatumia ujumbe wangu kwa mapokeo tofauti na wakatuvuruga"
Tangu arudi kutoka kwenye majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu, Kamusoko ameshindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mwinyi Zahera
Hata hivyo Mzimbabwe huyo bado ana uwezo mkubwa na amekuwa akidhihirisha hilo kila anapopewa nafasi na kocha Zahera