Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo saa kumi kamili jioni watakuwa dimba la Taifa wakipepetana na watani zao wa jadi, Yanga kwenye mchezo wa ligi
Baada ya kuifumua Al Ahly bao 1-0 Jumanne ya wiki hii, kikosi cha Simba kinachonolewa na kocha Patrick Aussems kilibaki jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo huo
Mabingwa hao wa kihistoria Afrika Mashariki wataingia kwenye mchezo huo wakiwa hawana hofu yoyote hasa baada ya matokeo mazuri dhidi ya Al Ahly
Kocha Aussems amesema wamefanya maandalizi ya kutosha, ana matumaini makubwa kuwa wachezaji watafanya kile alichowaelekeza ili waweze kushinda mchezo huo
"Mpango wa mchezo wetu ni kushambulia, hivyo nimewaelekeza wachezaji wangu watumie nafasi kufunga mabao ya mapema"
"Sitarajii changamoto ya mchezo wa kwanza ambao tulikosa mabao mengi, itajirudia katika mchezo wa kesho (leo)," alisema Aussems
Leo Aussems huenda akatumia kikosi kilichopata ushindi dhidi ya Al Ahly, ambapo nafasi ya Asante Kwasi aliyeumia katika mchezo huo itachukuliwa na Mohammed Hussein
Matokeo ya ushindi kwa Simba yatawaweka mabingwa hao watetezi kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao kwani kimahesabu, wataweza kuwazidi Yanga kwa alama tano
Baada ya mchezo wa leo Simba itaanza 'kupambana' na ratiba ya michezo ya viporo amapo Februari 19 itakwenda mkoani Arusha kuikabili African Lyon kisha kurejea jijini Dar es salaam kuikabili Azam Fc siku tatu baadae