Kikosi cha Simba tayari kimerejea nchini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuikabili AS Vital Club katika mchezo wa ligi ya mabingwa
Mchezo huo ambao ulipigwa juzi, uliishuhudia Simba ikikubali kipigo cha mabao 5-0.
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wapinzani wao walikuwa bora zaidi yao na kupitia mchezo huo amedhamiria kukiimarisha zaidi kikosi chake
"Wapinzani wetu walikuwa bora kwa timu na hata kwa mchezaji mmoja mmoja," alisema Aussems
"Vita wametuonyesha ni kwa kiwango gani tunahitaji kuwa imara ili tuweze kufanya vizuri wakati mwingine."
"Tunatakiwa kusahau haraka matokeo hayo na kuangalia michezo inayokuja mbele yetu. Bado tuna nafasi, tunaanza mara moja maandalizi ya mchezo unaofuta dhidi ya Al Ahly"
Simba itasafiri kwenda nchini Misri kuikabili Al Ahly katika mchezo utakaopigwa Februari 02 2019
Baada ya kurejea mabingwa hao wa Tanzania Bara wameingia kambini kujiandaa na mchezo wa robo fainali michuano ya SportPesa Super Cup dhidi ya AFC Leopards utakaopigwa keshokutwa Jumatano katika dimba la Taifa