Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema amekiandaa kikosi chake kikamilifu kuikabili Singida United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa
Aussems amesema kiufundi hana wasiwasi na wachezaji wake kazi iliyobaki ni kwao kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
"Tumejiandaa vizuri na hatuna wasiwasi kuelekea mchezo huo," amesema Aussems
"Tuna kikosi imara ambacho kinauwezo wa kutupa matokeo katika mchezo wowote wa ligi. Muhimu nimewaelekeza washambuliaji wangu wahakikishe wanatumia vyema nafasi ili tuweze kupata ushindi mnono"
Aussems na vijana wake wako katika presha kubwa ya kushinda mchezo wa kesho ili kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo ambao walikerwa na kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Mashujaa Fc kilichoiondoa mapema Simba kwenye michuano ya kombe la FA
Aidha Simba ambayo leo itawafahamu wapinzani wake wa hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, inahitaji kushinda ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wa ligi iliyotwaa msimu uliopita.
Katika mchezo wa kesho Aussems anatarajiwa kutumia kikosi chake kamili kilichoipeleka Simba hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.