Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, amepewa mbinu muhimu zitakazomsaidia kurejesha makali yake na kuanza kufungua akaunti ya mabao katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Doumbia, aliyesajiliwa na Simba mwezi Julai akitokea AS Korofina ya Mali, amekuwa akikabiliwa na presha baada ya kushindwa kufunga tangu kuanza kwa msimu mpya, katika mechi za Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Tangu atue Msimbazi, Doumbia amefunga bao moja tu kwenye michuano ya CECAFA iliyofanyika nchini Rwanda mwishoni mwa mwezi Julai 2026.
Wachambuzi wa soka wanaona kuwa mshambuliaji huyo bado hajafanikiwa kuendana kikamilifu na kasi pamoja na mfumo wa timu, tofauti na baadhi ya nyota wenzake ambao wamekuwa wakisaidia kufanya mashambulizi ya Simba kuwa na kasi na mabadiliko ya haraka.
Doumbia atakiwa kubadili mtindo wa uchezaji
Moja ya mambo makubwa aliyoshauriwa Doumbia ni kubadili namna anavyocheza ili kuendana na mfumo wa timu, badala ya kuifanya Simba ibadilishe namna yake ya kucheza ili kumfuata yeye.
Mshambuliaji huyo anatakiwa kuelewa vizuri majukumu yake ndani ya mfumo wa Kocha Mkuu, Steve Barker, na kutumia nafasi zinazotengenezwa na wachezaji wenzake.
Hii itamsaidia kuwa sehemu ya mfumo wa timu badala ya kuwa mchezaji anayesubiri timu imtengenezee mazingira maalumu ya kucheza.
Utulivu mbele ya lango
Doumbia pia ametakiwa kuwa na utulivu zaidi anapofika kwenye eneo la hatari.
Presha ya kufunga bao la kwanza inaweza kumfanya mshambuliaji kufanya maamuzi kwa haraka au kulazimisha mambo. Kwa hiyo, anatakiwa kuwa mtulivu, kuamini uwezo wake na kutumia nafasi anazopata kwa umakini zaidi.
Bao la kwanza linaweza kuwa muhimu katika kumrudishia hali ya kujiamini, hasa baada ya kuanza msimu bila kufunga.
Kuongeza juhudi uwanjani
Mbali na suala la mabao, Doumbia anatakiwa kuongeza work rate yake katika kipindi chote cha mchezo.
Hii inahusisha kufanya presha kwa mabeki wa wapinzani, kukimbia bila mpira, kutafuta nafasi nyuma ya mabeki na kuwa tayari kuitumia kila nafasi inayotengenezwa na viungo pamoja na mawinga.
Kwa kufanya hivyo, ataweza kuwa sehemu muhimu zaidi ya mfumo wa Simba hata pale ambapo hafungi.
Mshambuliaji huyo amekiri kuwa anapitia kipindi cha mpito, lakini amesema yuko tayari kupambana ili kurejesha imani ya mashabiki wa Simba.
βNatambua matarajio ya mashabiki na ninajua napitia wakati mgumu, lakini ninafanya kazi kwa bidii kila siku. Nitapambana na kutoa kila nilichonacho ili kuisaidia timu yangu kupata matokeo,β alisema Doumbia.
Barker bado anamwamini
Pamoja na ukame wa mabao, benchi la ufundi chini ya Steve Barker limeendelea kumpa nafasi Doumbia, jambo linaloonyesha kuwa bado anaaminiwa ndani ya kikosi.
Kwa sasa, changamoto kubwa kwake ni kubadilisha nafasi anazopata kuwa mabao na kuanza kuonyesha matokeo ya usajili wake.
Wakati huu ambao ligi imesimama kupisha kalenda ya FIFA pengine ni wakati sahihi kwake kujiimarisha zaidi na kuhakikisha anarejea na makali mapya pale ligi itakapoendelea kwa mchezo wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga Oktoba 10.