Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema kukosekana kwa muda mrefu wachezaji Yacouba Songne na Saido Ntibazonkiza kulichangia timu yake kupoteza mwelekeo tangu kuanza kwa duru la pili Ligi Kuu ya Vodacom
Wiki iliyopita uongozi wa Yanga ulitangaza kumfuta kazi Kaze na benchi lake la ufundi baada ya mfululizo wa matokeo mabaya
Kaze amejitetea kuwa timu yake ilikabiliwa na changamoto za hapa na pale ikiwemo kukosekana kwa wachezaji hao muhimu
"Huwa sipendi sana kuzungumzia mchezaji mmoja mmoja, lakini kwa hali iliyopo kwenye kikosi kwa sasa nguvu ya Saido na Yacouba inahitajika sana, ni wachezaji ambao wana uzoefu mkubwa na wakiwepo wanaongeza morali kikosini," Kaze alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Kocha huyo raia wa Burundi amesema kocha ajaye inaweza kuwa na changamoto ileile aliyokutana nayo na pengine kuathiri mbio zao za ubingwa kama nyota hao hawatarejea wakiwa kwenye ubora wao
"Safari ya ubingwa inaweza kuwa ngumu kidogo, kwani wachezaji hawa wakiwa kwenye timu unaona kabisa na kiwango cha kujiamini kwa baadhi ya wachezaji kinapanda zaidi na unaona timu inacheza kwa nguvu zaidi, vitu kama hivyo ni muhimu zaidi kwenye timu kuelekea kwenye safari ya ubingwa muda kama huu
Yacouba tayari amerejea kikosini akipata nafasi ya kucheza dakika kadhaa katika mechi zilizopita wakati hali bado ni tete kwa Ntibazonkiza ambaye haijafahamika ni lini atarejea kikosini
Ntibazonkiza yuko nje ya uwanja tangu mwezi Januari baada ya mchezo wa fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba
Nyota huyo anasumbuliwa na uvimbe nyuma ya goti ikielezwa hali yake inaendelea vizuri
Amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi ambayo itacheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afcon 2021 hapa Tanzania mwishoni mwa mwezi huu
Kabla hajatimuliwa, Kaze alipinga Ntibazonkiza na Dickson Job kuitwa timu za Taifa kwa kuwa afya zao zilikuwa hazijatengememaa sawasawa
Job amejumuishwa kwenye kikosi cha Tanzania ambacho kiko kule Kenya kwa ajili ya mechi mbili za Kimataifa za kirafiki dhidi ya Harambee Stars