Wananchi wanaweza kufanya makosa makubwa kama watakata tamaa na mbio za ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Ukitizama ushindani uliopo, ni wazi mpaka sasa hakuna timu ambayo inaweza kusema inajihakikishia itashinda ubingwa huo pamoja na kuwa ushindani mkubwa unazihusisha Yanga na Simba, hapa Azam wanaweza kufanya kitu
Yanga ina faida ya kuwa kileleni baada ya kujikusanyia alama 50 kutokana na michezo 23 waliyocheza
Watani zao Simba wana alama 46 kutokana na michezo 20 waliyocheza, bado wana mechi tatu za viporo
Sio kila siku timu ikiwa na viporo basi inashinda vyote, msimu huu mambo yanaweza kuwa tofauti sana
Timu zilizo katika ushindani wa kuteremka daraja ni nyingi hivyo hazitakuwa tayari kugawa alama kirahisi
Yanga wameshindwa kupata ushindi katika michezo yao minne waliyocheza ugenini katika duru ya pili, ni kutokana na ushindani mkubwa waliokutana nao
Pamoja na kuwa matokeo hayo yalipelekea benchi la ufundi kuvunjwa, lakini ni ishara kuwa ushindani ni mkubwa, kila timu imejipanga kupata matokeo inapocheza nyumbani
Jana Simba nao wameponea chupuchupu mbele ya Tanzania Prisons, wakirejesha bao kwenye dakika za lala salama, tena bao ambalo wengi wanaamini mfungaji alikuwa ameotea
Walicheza na Prisons ambayo muda mwingi ilikuwa na wachezaji pungufu baada ya mchezaji wao mmoja kupewa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza
Lakini chupuchupu wapate alama nyingine tatu dhidi ya Simba msimu huu. Hii ni ishara ya aina ya ushindani ambao tutausuhudia katika mechi hizi za kukamilisha duru ya pili
Muhimu kwa Yanga, kocha Juma Mwambusi ahakikishe anakiimarisha kikosi ili kupunguza makosa ambayo yalipelekea Yanga kupoteza alama katika mechi walizokuwa wanakaribia kuondoka na ushindi mfano mechi dhidi ya Mbeya City na hivi karibuni dhidi ya Polisi Tanzania