Ni kipigo cha kwanza msimu huu kwa Yanga baada ya kukubali kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopigwa uwanja wa Mkwakwani
Vijana wa Coastal Union walistahili ushindi huo kwani walikuwa bora zaidi kuliko Yanga ambayo leo ilikuwa chini sana
Tuisila Kisinda alipoteza nafasi ya kuipa uongozi Yanga mapema tu baada ya kukosa mkwaju wa penati lakini dakika mbili baadae,kinda aliyelelewa na Yanga Erick Msagati akaifungia Coastal Union bao la uongozi
Kisinda alisahihisha makosa yake kwa kuirejesha Yanga mchezo mwishoni mwa kipindi cha kwanza
Coastal Union walirejea wakiwa imara zaidi kwenye kipindi cha pili, bao la pili waliliweka kambani kwenye dakika ya 84, Mudathir Said akifunga kwa shuti la chinichini lililomshinda Farouk Shikhalo
Ni matokeo yatakayowaumiza sana Wananchi lakini kwa hakika, safari ya ubingwa kwa Yanga yetu hii ni ngumu, kwani kikosi kinaporomoka kiwango siku hadi siku
Kimahesabu kama Simba watazichanga karata zao vyema, wakashinda mechi zao zote za viporo, watakaa kileleni kwa tofauti ya alama tano
Bado mechi ni nyingi, kukata tamaa sasa ni makosa, lakini kwa hakika lazima wachezaji wa Yanga wakae chini na benchi la ufundi pamoja na viongozi kusaka suluhu haraka