Timu ya Wananchi Yanga iko mkoani Tanga ambapo keshokutwa Alhamisi watashuka katika uwanja wa Mkwakwani kuikabili Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Huu ni mchezo muhimu kwa Yanga ambayo itakuwa na jukumu la kumaliza unyonge ndani ya Mkwakwani kwani tangu mwaka 2015, Wananchi hawajaondoka na alama zote tatu
Jana kupitia mitandao ya kijamii, viongozi wa Coastal Union walitamba kuwa wanakwenda kumaliza ubabe wa Yanga kwenye ligi kwa kuwa timu ya kwanza kupata ushindi dhidi ya mabingwa hao wa kihistoria msimu huu
Hata hivyo kwa wachezaji wa Yanga, wanafahamu huu ni mchezo muhimu sana kwao kupata ushindi ili kuendelea kujiimarisha kileleni
Matokeo tofauti na ushindi kwa Yanga, yatatoa faida kwa Simba ambayo itakuwa na michezo mitatu ya viporo huku wakihitaji alama nne tu kuiondoa Yanga katika uongozi wa ligi
Hili linaweza kuwaongezea presha wachezaji wa Yanga katika michezo yao inayofuata ambapo wakitoka mkoani Tanga watasafiri Kilimanjaro kuifuata Polisi Tanzania
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema timu imewasili salama mkoani Tanga, ari ya wachezaji iko juu wakitarajia kupata sapoti nzuri kutoka kwa mashabiki wao
Nae Afisa Mhamasishaji Antonio Nugaz amesema wamezisikia tambo za Coastal Union lakini amewaambia majibu watayapata Alhamisi jioni baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika