Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga, jioni ya leo Jumamosi watashuka katika uwanja wa Uhuru kumenyana na Kengold ukiwa ni mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) raundi ya nne
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kushuka dimbani katika michuano hiyo msimu huu, raundi iliyopita wakivuka pasipo kushuka uwanjani baada ya Singida United kushushwa daraja
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema vijana wako wako tayari kuwapa furaha mashabiki wao lengo likiwa kushinda na kuvuka hatua inayofuata
"Nafikiri hautakuwa mchezo mwepesi kama watu wengi wanavyofikiria. Sisi tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunpata matokeo mazuri tuweze kuvuka hatua inayofuata. Kila mchezo kwetu ni muhimu hivyo hatutawadharau wapinzani wetu," alisema Kaze
Wachezaji wa Yanga leo wataingia katika mchezo huo wakiwa 'fresh' kwani wamepata takribani wiki moja ya kujifua tangu wacheze mechi ya ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita
Mchezo utapigwa kuanzia saa kumi kamili Alasiri