Nyota wa klabu ya Yanga wametamba kuwa wataibuka ushindi katika mchezo wa raundi ya nne kombe la FA dhidi ya Kengold ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Uhuru
Akizungumza jana Kigamboni katika mazoezi ya vinara hao wa ligi kuu, Deus Kaseke amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo
"Sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda. Ari ya wachezaji iko juu kila mmoja yuko tayari kwa ajili ya mchezo huo, tunasubiri muda ufike. Hautakuwa mchezo mwepesi lakini nadhani tutashinda," alisema Kaseke ambaye ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga
Nae kiungo fundi Feisal Salum 'Fei Toto' amesema kuwa wanafahamu Kengold watakamia mchezo huo, lakini wao hakuna jambo jingine wanahitaji zaidi ya ushindi
"Hautakuwa mchezo mwepesi, kwa wapinzani wetu huu ni mchezo mkubwa kwao, watataka kuonyesha uwezo wao lakini nasi tumejipanga vizuri muhimu tusubiri dakika 90 zitaongea," alisema
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kwenye michuano ya FA msimu huu wakivuka raundi iliyopita bila ya kushuka dimbani baada ya wapinzani wao Singida United kushushwa madaraja mawili hivyo kukosa sifa ya kushiriki michuano hiyo
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema wameipa michuano hii kipaumbele kama ilivyo ligi kuu. Hivyo ni mchezo ambao wanahitaji kushinda ili wasonge mbele hatua inayofuata