Yanga imeshindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa tatu mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Makosa yaliyofanyika katika kipindi cha kwanza ndio yaliyogharimu Yanga leo kwa kuruhusu mabao matatu rahisi sana
Peter Mwalyanzi aliitanguliza Kagera Sugar kwa bao la mapema kwenye dakika ya 11 kabla ya Tuisila Kisinda kuisawazishia Yanga dakika tatu baadae kupitia mkwaju wa penati
Mwaterema akaweka kambani bao pili la Kagera Sugar kwenye dakika ya 24, Deus Kaseke akakomboa bao hilo kwenye dakika ya 30
Mtoto wa nyumbani Yusufu Mhilu akafunga bao la tatu dakika za majeruhi kuelekea mapumziko
Mukoko Tonombe ambaye mchezo wa leo alianzia benchi, aliirejesha Yanga mchezoni kwenye dakika ya 61 akifunga bao kwa shuti kali kutoka nje ya 18
Yanga ilitawala kipindi cha pili lakini haikufanikiwa kupata bao la ushindi licha ya kutengeneza nafasi nyingi
Ditram Nchimbi alikosa nafasi adimu dakika za majeruhi huku Yanga ikinyimwa mkwaju wa penati katika muda wa nyongeza
Kocha Cedric Kaze amesema makosa ya kiufundi waliyofanya kwenye kipindi cha kwanza ndio yaliyowagharimu
Mabadiliko aliyofanya wakati wa mapumziko kwa kuwatoa Zawadi Mauya na Michael Sarpong nafasi zao kuchukuliwa na Mukoko na Nchimbi, yaliifanya Yanga iwe imara katika kipindi hicho
Yanga inatarajiwa kushuka tena uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi Februari 20 kuikabili Mtibwa Sugar