Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza afya yake imeendelea kuimarika na pengine anaweza kurejea uwanjani mapema kuliko ilivyodhaniwa
Nyota huyo anasumbuliwa na uvimbe nyuma ya goti, taarifa iliyotolewa awali ikibainisha kuwa anaweza kukaa nje kwa wiki nne au zaidi
Hata hivyo Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema afya ya Ntibazonkiza imeendelea kuimarika na Wananchi wamtarajie kumuona uwanjani siku sio nyingi
Carlinhos yuko fit
Kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa baadae leo, Nugaz amethibitisha kuwa kiungo Carlos Carlinhos yuko imara kwa ajili ya mchezo huo na ikimpendeza, Kocha Cedric Kaze anaweza kumpa nafasi leo
Carlinhos hakuwa sehemu ya kikosi kilichoshuka dimbani katika mchezo uliopita mkoani Mbeya Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City
Pengine Kaze alihofia kumtumia katika mchezo huo kutokana na mazingira yake. Ulikuwa mchezo wa matumizi makubwa ya nguvu na uwanja haukuwa rafiki
Carlinhos amerejea kikosini hivi karibuni baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa takribani miezi mitatu