Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga leo wana jambo lao pale uwanja wa Benjamin Mkapa watakaposhuka uwanjani kuwakabiri Kagera Sugar katika mchezo wa kukata na shoka
Mapema kabla ya mchezo huo, Yanga itakuwa na tukio la maadhimisho ya miaka 86 ya mabingwa hao wa kihistoria
Mchezo wenyewe unatarajiwa kupigwa kuanzia saa moja usiku wakati maadhimisho ya miaka 86 ya Yanga hafla itaanza hapa hapo kwa Mkapa kuanzia saa 11 jioni
Baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopita, huu ni mchezo ambao Yanga inahitaji kuondoka na alama zote tatu
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi kwa Wananchi, wachezaji watapaswa kupambana kwelikweli ili kupata matokeo
Kagera Sugar inayonolewa kocha Mecky Mexime imekuwa na kawadia ya kutoa upinzani mkali kwa Yanga katika mechi ambazo zinapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Msimu uliopita Kagera Sugar walishinda mabao 3-0 kabla ya Yanga kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali kombe la Shirikisho
Ulikuwa ushindi ambao ulipatikana kwa taabu sana
Msimu huu Yanga iliuanza kwa kuondoka na alama zote tatu katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Kaitaba, Kagera wakati huo Yanga ikinolewa na Zlatko Krmpotic
Kwa Kocha Cedric Kaze, huu utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar
Malengo ya Yanga msimu huu ni kushinda ubingwa, hivyo kwa duru hii ya pili, ni muhimu sana kwa Wananchi kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuondoka na alama zote tatu kwenye kila mchezo