Baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City juzi, Yanga ilirejea jijini Dar es salaam jana na moja kwa moja kuelekea kambini kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya kagera Sugar utakaopigwa keshokutwa Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga imethibitisha muda wa mchezo huo kuwa ni saa moja usiku
Huu ni mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, Yanga inahitaji kuwa katika ubora hasa ili kuondoka na alama zote tatu
Kwa misimu ya karibuni, Kagera Sugar imekuwa ikiipa changamoto sana Yanga kwa michezo inayochezwa uwanja wa Benjamini Mkapa licha ya kuwa mabingwa hao wa kihistoria wameendelea kutamba mechi zilizopigwa Kaitaba, Bukoba
Mchezo wa duru ya kwanza uliishuhudia Yanga ikiondoka na ushindi wa bao 1-0 na sasa Jumatano wanahitaji kurudia kile walichokifanya Kaitaba
Aidha sare ya Mbeya City inaifanya Yanga kulazimika kushinda mchezo huo ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu hesabu zake zikiwa kushinda ubingwa
Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, Kocha Cedric Kaze aligoma kuwapa wachezaji wake mapumziko baada ya kurejea kutoka Mbeya, kikosi kiliingia kambini na kuendelea na program za mazoezi
Licha ya kuacha alama mbili mkoani Mbeya, Kaze amesisitiza kuwa lengo la kushinda ubingwa bado liko palepale