Somo moja ambalo kocha Cedric Kaze amelipata katika mchezo dhidi ya Mbeya City jana, ni kuwa Deus Kaseke ndiye mchezaji muhimu sana katika safu yake ya ushambuliaji
Kaseke anapaswa kuendelea kuwa katika kikosi chake cha kwanza kwani amedhihirisha kila mara anapokuwa uwanjani anaweza kusababisha jambo
Hapa tunamzungumzia kiungo mshambuliaji ambaye ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha Yanga akiwa amefunga mabao matano
Katika mchezo dhidi ya Mbeya City , Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya Kaseke kuingia
Naamini kama angekuwepo uwanjani tangu kipindi cha kwanza, pengine Yanga ingefunga mapema tu
Kuna nafasi nyingi zilipotezwa katika kipindi cha kwanza, Yanga ingeweza kumaliza mchezo mapema sana kama kina Feisal, Sarpong na Fiston wangekuwa makini katika nafasi adimu walizopata
Lakini dakika 20 alizocheza Kaseke zilikuwa na thamani zaidi kwani alifunga bao pekee la Yanga
Pia kama mwamuzi angekuwa muungwana, kulikuwa na mkwaju wa penati ambao Yanga walistahili kupewa baada ya Kaseke kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari
Kaze pia atakuwa amepata somo kuwa anao wachezaji ambao anapaswa kuwatumia katika baadhi ya mechi ngumu hasa hizi za mikoani zinazochezwa katika viwanja 'korofi'
Ditram Nchimbi, Deus Kaseke na hata Waziri Junior ni aina ya wachezaji hao
Mshambuliaji Fiston Abdul Razak haukuwa mchezo mzuri sana kwake kuanza mkoani Mbeya
Bado hajazoeana na wenzake lakini pia hafahamu mazingira ya viwanja vyetu mikoani, mchezo ule ulikuwa wa kwanza kwake nje ya jiji la Dar es salaam
Kuingia kwa Nchimbi kuliongeza presha kwa walinzi wa Mbeya City, ni mchezaji anayefahamu kulazimisha
Yanga bado ina timu imara yenye uwezo wa kushinda ubingwa, changamoto zinazojitokeza zirekebishwe tu ili kuhakikisha idadi ya sare ambazo timu inapata haziathiri lengo kuu la kushinda ubingwa