Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano klabu ya Yanga Injinia Hersi Said amesema wamekubali matokeo ya mchezo dhidi ya Mbeya City na wanarudi kujipanga kwa ajili ya mechi zinazofuata
Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Sokoine jioni ya leo
Hersi ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, amesema yeye sio kazi yake kuzungumzia masuala ya waamuzi, jambo la msingi wanakwenda kujipanga ili kuhakikisha wanasahihisha makosa katika mchezo unaofuata
"Sote tumeuona mchezo ulivyochezwa, siwezi kumnyooshea kidole mtu yoyote, kilichotokea kimetokea ni sehemu ya mchezo. Muhimu kwetu tumekubali matokeo, tunarejea kujipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata"
"Ligi ni kama mbio za marathon baada ya mchezo mmoja kumalizika unakuja mchezo mwingine," alisema Hersi
Yanga inarejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya mechi mbili za ligi dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar