Katika mechi za mwanzoni mwa msimu, Carlos Carlinhos ndiye mchezaji aliyekuwa akizungumzwa sana na mashabiki wa Yanga
Katika michezo mitano ya kwanza, wakati huo Yanga ikinolewa na Zlatko Krmpotic, Carlinhos ndiye aliyekuwa 'jiko' la kupika mabao
Aliisaidia Yanga kupata ushindi katika mazingira ambayo wengi walikuwa wamekata tamaa
Matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City yanakumbukwa. Kona yake ya dakika ya 87 iliwekwa kambani na nahodha Lamine Moro hivyo kuisaidia Yanga kuondoka na alama zote tatu jijini Dar es salaam
Pia alifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, baadae akaja kuhusika tena katika mchezo dhidi ya Coastal Union, mchezo ambao alifungua akaunti yake ya mabao akifunga pia katika mchezo dhidi ya Namungo Fc
Lakini baada ya mechi hizo, Carlinhos akapotezwa na majeraha ya nyama za paja yaliyomsumbua kwa karibu miezi mitatu
Sasa amerejea tena kikosini, mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports akicheza nusu yote ya pili
Amerejea wakati ambao Wanayanga wanamkosa Saido Ntibazonkiza ambaye anasumbuliwa na matatizo ya misuli
Kurejea kwake ni ahueni kwa Yanga, kwani anatarajiwa kukabidhiwa majukumu yote aliyokuwa akiyafanya Ntibazonkiza
Kama ilivyo kwa Ntibazonkiza, Carlinhos ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao kupitia mipira yake ya adhabu na krosi
Hii ni silaha muhimu sana kwa Yanga hasa kwa hizi mechi zinazochezwa mikoani