Kikosi cha Yanga kiliwasili mkoani Mbeya jana jioni kuelekea mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kesho Jumamosi, uwanja wa Sokoine
Akizungumza baada ya kuwasili, Mkuu wa Msafara Said Khimji amesema wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu
"Tumekuja Mbeya na msafara wa wachezaji 24, benchi la ufundi wanane na viongozi tuko sita. Kilichotuleta hapa ni kusaka ushindi dhidi ya Mbeya City"
"Nakumbuka msimu uliopita tulikuja hapa katika kipindi kama hiki cha baridi, hatukufanikiwa kupata ushindi dhidi ya Mbeya City ingawa tuliweza kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Prisons"
"Safari hii tumejipanga, hatutarudia makosa, vijana wako vizuri na wana ari, matumaini ya ushindi ni makubwa," alisema Khimji
Mabingwa hao wa kihistoria leo watakamilisha maandalizi yao ya mwisho katika uwanja wa Sokoine tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi kuanzia saa kumi kamili jioni