Mshambuliaji Fiston Abdul Razak mwishoni mwa wiki alipata nafasi ya kuitumikia Yanga kwa mara ya kwanza katika mchezo wakirafiki dhidi ya African Sports
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Azam Complex Chamazi, uliishuhudia Yanga ikipoteza kwa mara ya kwanza baada ya kucheza zaidi ya michezo 40 bila kufungwa
Kwa Fiston pia haikuwa siku nzuri sana, kwani ugeni wake kikosini ulidhihiri, bado hajawa na muunganiko mzuri na wachezaji wenzake
Katika mchezo huo Fiston alipatikana katika eneo la kuotea mara tano. Ni wazi bado viungo wa Yanga hawajafahamu vile wanaweza kumpasia kwa wakati
Habari njema ni kuwa fundi Saido Ntibazonkiza yuko mbioni kurejea kikosini
Ntibazonkiza anamfahamu zaidi Fiston kwani wamecheza pamoja katika timu ya Taifa kwa muda mrefu

Kwa aina ya pasi ambazo Ntibazonkiza amekuwa akipiga, ni wazi kurejea kwake kutamnufaisha Fiston ambaye hupendelea kupigiwa mipira mbele yake akimbizane na mabeki
Tofauti na washambuliaji wengi, Fiston sio mchezaji anayependa kupokea mipira akiwa amelipa mgongo goli
Utaona kwa nini mchezo dhidi ya African Sports aliotea sana. Ni kwa sababu viungo wa Yanga walishindwa kwendana na kasi yake na kuchelewa kumpasia mipira
Yanga imekuwa na changamoto eneo la kiungo cha uchezeshaji, Ntibazonkiza amejipambanua kwa kuonyesha utofuti katika eneo hilo
Lakini pia kurejea kwa Carlinhos ni faida kwa Yanga kwani nae ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi na mipira yenye madhara katika lango la timu pinzani
Katika mchezo dhidi ya African Sports Yanga ingeweza kufunga mabao mengi kwenye kipindi cha pili kama mipira yake ya adhabu ingetumika vizuri