Wakati mabosi wa Yanga wakimleta Edem Mortotsi kuwa kocha wa viungo pamoja na utimamu wa mwili nafasi ambayo ilikuwa wazi tangu kuondoka kwa Riedoh Berdien raia wa Afrika Kusini, Kocha Mkuu wa vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Cedric Kaze, amesema maboresho waliyofanya yatawaongezea nguvu kwenye mbio za ubingwa msimu huu
Mortotsi aliyekuwa akiichezea klabu ya FC Edmonton ya Canada, alitambulishwa jana kuwa kocha wa viungo sambamba na kiungo wa zamani wa Yanga Nizar Khalfan anayekuwa Kocha Msaidizi

Kaze amesema ujio wa wataalam hao pamoja na usajili uliofanyika wakati wa dirisha ulikuwa wa malengo na anaamini kasi waliyoionyesha katika mzunguko wa kwanza wataiendeleza.
Kocha huyo wa zamani Academy ya Fc Barcelona, amesema Yanga ina jambo moja tu msimu huu nalo ni kuwavua Simba ubingwa, hivyo akili, mikakati na mipango yao ni kufanya vema katika mechi zote zilizobaki kwenye duru ya pili
"Tunaendelea vizuri na mazoezi na wachezaji wote wanajua malengo ya timu, kila mmoja anapojiunga na Yanga anajua amekuja kuongeza nguvu, naamini tutatimiza ahadi hii, ingawa hakuna kazi rahisi kwenye mbio hizi," alisema Kaze.
Kaze aliongeza kuwa anatarajia upinzani mkali kutoka kwa timu za Simba na Azam Fc katika mbio za ubingwa hivyo jambo la msingi kwao ni kuhakikisha wanafanya vizuri mechi zao
"Ubingwa hauna mwenyewe, kikubwa sisi tushinde mechi zetu, huwezi kuwa bingwa kama wewe mwenyewe unafanya vibaya, tunajaribu kurekebisha makosa ili ligi itakaporudi tuwe tumeimarika na tayari kupambana"