Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi ambaye jana aliomba kupumzika majukumu yake ndani ya klabu kutokana na matatizo ya kiafya, anatarajiwa kuanza matibabu yake Hospitali ya Muhimbili Jumatatu
Mwambusi amebainisha kuwa anasumbuliwa na jino kwa muda mrefu na kupata maumivu makali ya kichwa.
Amekuwa akitumia dawa bila ya kupata nafuu, hivyo akalazimika kurudi Hospitali ya taifa ya Muhimbili, ambako ameshauriwa kufanyiwa upasuaji mdogo.
Alisema anatarajiwa kufanyiwa operesheni ndogo Jumatatu ya Januari 25, mwaka huu, kwa ajili ya kutenganisha mshipa mdogo na jino.
"Baada ya vipimo iligundulika kwamba, nina matatizo katika mfumo wa meno, mshipa wa kichwa umeungana na jino, ndio imeleta tatizo kubwa na jopo la daktari limenishauri nipumzike kidogo na kazi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo, kutenganisha mshipa huo na jino," alisema Mwambusi.
"Jumatatu natarajiwa kufanyiwa upasuaji huo mdogo, hivyo sitaweza kujihusisha na timu, endapo nitashauriwa kuachana kabisa na soka basi nitalazimika kukaa pembeni na kufanya shughuli zingine," aliongeza
Jana Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alithibitisha kupokea barua ya Mwambusi akiomba kujiweka kando akitaja sababu ni matatizo ya kiafya
Yanga huenda italazimika kujaza nafasi yake ambapo kocha wa African Lyon, kiungo wa zamani wa Yanga Nizar Khalfan anatajwa kuwa mbioni kujiunga mabingwa hao wa kihistoria