Mshambuliaji wa Yanga Yacouba Songne amerejeshwa Hospitalini kufanyiwa uchunguzi zaidi wa jeraha la nyama za paja linalomsumbua mara kwa mara
Yacouba aliumia kwenye mchezo wa nusu fainali michuano ya kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam Fc hivyo akakosa mchezo wa fainali dhidi ya Simba
Daktari wa Yanga Dk Shecky Mngazija amesema nyota huyo raia wa Burkina Faso, anafanyiwa uchunguzi wa kina kubaini tatizo linalomsumbua
"Yacouba tumempeleka tena hospitali ili kumfanyia vipimo vingine zaidi kufahamu shida ambayo inamsumbua ni ipi na kwa nini ameshindwa kupona katika matibabu ya awal"
"Baada ya hapo ndio ataanza tiba mpya na kufahamu atakuwa nje kwa muda gani," amesema
Carlinhos yuko sawa
Katika hatua nyingine, Dk Mngazija amesema kiungo Carlos Carlinhos ameanza mazoezi mepesi baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu
Nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichokuwa Zanzibar kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi lakini alirejeshwa jijini Dar es salaam mapema baada ya kujitonesha majeraha
Dk Mngazija amesema Carlinhos alichanika nyama za paja lakini pia akapata uvimbe mbele ya paja la kulia. Nyota huyo hali yake inaendelea vizuri akiwa tayari ameanza mazoezi mepesi