Habari za uhakika ni kuwa wachezaji wa Yanga wamepata mgawo wao kutoka kwa wadhamini GSM baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya kombe la Mapinduzi
GSM waliweka mezani kitita cha Tsh Milioni 300, kwa ajili ya ubingwa lakini muhimu zaidi ilikuwa kwa ajili ya ushindi dhidi ya Simba
Baada ya kutua jijini Dar es salaam kutoka Zanzibar walikotwaa taji hilo, Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said alisema wachezaji walistahili zawadi kubwa kutokana na kujitoa kwao kwa ajili ya kuipambania timu
"Tunatambua mchango mkubwa wa wapambanaji wetu ambao wametupa heshima kubwa ya Kombe la Mapinduzi, kama watu wataliona hili ni kombe dogo basi watambue baada ya hili makubwa mengine yatakuja kupitia hawahawa wapambanaji wetu," alisema Hersi
Tangu walipoanza kuidhamini Yanga msimu uliopita, GSM wametumia utaratibu huo wa kuwahamasisha wachezaji kuhakikisha wanafanya vizuri na kuwatuza pale wanapofanikisha malengo yaliyowekwa