Baada ya Yanga kurejea na Kombe la Mapinduzi, kesho Jumatatu, mmoja wa wadhamini wao GSM ameahidi kuwapa wachezaji wote walioshiriki michuano hiyo na kurudi mashujaa zawadi nono
Yanga ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Simba kwa penalti 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar hivi karibuni
Akizungumza baada ya kikosi hicho kurejea Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said alisema wachezaji hao ni wanaume katika wanaume kutokana na kile walichokifanya kwenye michuano hiyo.
"Sisi wadhamini Jumatatu tutakabidhi zawadi nono mashujaa wetu," alisema Hersi na kuongeza kuwa wataendelea kushirikiana na klabu hiyo katika kujenga kikosi chenye ushindani
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Cedric Kaze aliwasifu wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichokionesha katika michuano hiyo kwani wamefanya kazi yake ionekane rahisi.
"Kama una wachezaji wa hivi huwezi kuwa na kazi ngumu, tunajua bado hatujamaliza kazi, tunahitaji kupambana katika michuano ijayo ili tuifanye vizuri zaidi, " alisema
Kaze alisema kwa sasa mashabiki wa klabu hiyo wanaweza kutembea kifua mbele na kuvaa jezi zao kwani huko nyuma walikosa ujasiri kwa sababu ya kukosa kombe