Mshauri na Msimamizi wa mchakato wa Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji klabu ya Yanga, Senzo Mazingisa amesema anaendelea na majukumu yake katika klabu ya Yanga baada ya kumaliza likizo ya muda mfupi
Senzo alipewa likizo ya muda mfupi akarejea kwao Afrika Kusini kuiona familia katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Senzo amemjibu msemaji wa Simba Haji Manara aliyekuwa anajaribu kuanzisha upotoshaji wa taarifa kuwa Senzo ameondolewa Yanga
"Niko vizuri na salama kabisa rafiki yangu (Manara), nashukuru kwa kunikumbuka lakini una namba yangu ya simu ungeweza kunipigia au ulikuwa ukisubiri ruhusa kutoka kwa Trump!," aliandika Senzo
"Najua hutaki shida huko uliko, nakutakia kheri ya mwaka mpya. Mimi niko kazini ndugu yangu, nilipewa likizo ya muda mfupi kuona familia, gharama za likizo yangu zililipwa na Bosi wetu (mimi na wewe) hivyo usiwe na shaka nami"
"Sisi tunaendesha klabu ya mpira Yanga Sc na sio timu ya Mpira! Mimi nahusika zaidi na mambo ya msingi kama mchakato wa Mabadiliko wenye uwazi hapa Tanzania. Karibuni nitatangaza tarehe ya kuanza kwa Mwananchi Marathon tukio ambao litafanyika hivi karibuni," aliongeza Senzo
Inaelezwa Haji Manara nae ni mwajiriwa wa GSM akipewa dili mbalimbali za kutangaza bidhaa za GSM zikiwemo jezi za klabu ya Yanga, kazi ambayo anaifanya vizuri sana katika kurasa zake za mitandao ya kijamii. Ndio maana hata Senzo amedokeza kuwa gharama za likizo yake zililipwa na Bosi wao yeye na Manara
Aidha, Baada ya kufunga ndoa hivi karibuni, GSM walimzawadia Manara gari jipya lakini pia wakagharamia 'fungate' lake
Ni huyuhuyu Haji Manara ambaye baba yake Mzee Sunday Manara ni Mwanayanga kindakindaki aliyeitumikia Yanga akiwa mchezaji na hata baadae kupewa majukumu ya kiuongozi!