Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amewashukuru wenzake wa benchi la ufundi baada ya kutangazwa kuwa kocha bora wa mwezi Disemba 2020, ligi kuu ya Vodacom
Kaze aliyejiunga na Yanga katikati ya mwezi Oktoba, hiyo ni tuzo yake ya pili
Kocha huyo raia wa Burundi amesema kuwa ni faraja kwake kushinda tuzo hiyo, hata hivyo hakuwa peke yake
"Ni faraja kubwa kwangu kushinda tuzo hii lakini peke yangu nisingeweza, nimeshinda kwa ushirikiano wa benchi la ufundi. Nawashukuru kocha Juma Mwambusi, Hafidh Saleh, Jaco Farid, Dk Sheck Mngazija bila ya kuwasahau wachezaji wote"
"Hii ni heshima kwetu Yanga na benchi lote la ufundi," alisema Kaze
Wakati Kaze akitangazwa kushinda tuzo hiyo, kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza yeye alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Disemba
Kwa Disemba, Saido aliwashinda kiungo Clatous Chama wa Simba na kiungo mshambuliaji wa Dodoma Jiji FC, Seif Karihe alioingia nao fainali
Saido alionesha uwezo mkubwa katika michezo mitatu aliyocheza na kuwa msaada mkubwa kwa Yanga, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho tatu zilizozaa mabao
Saido amesajiliwa Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa katikati ya mwezi uliopita.