Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema pamoja na kuwa timu yake haikuweza kupata ushindi dhidi ya Jamhuri Fc jana, vijana wake wamenufaika na mchezo huo
Kikosi cha Yanga kililazimishwa suluhu ya bila kufungana na vijana wa Jamhuri ambao msimu huu wanashiriki ligi daraja la kwanza kule visiwani Zanzibar
Akizungumza baada ya mchezo huo uliopigwa usiku, Kaze alisema vijana wake wametoka kwenye ratiba ngumu ya mechi za ligi hivyo ilikuwa ni lazima kufanya mabadiliko ya kikosi chake
"Tulikuwa mkoani kwa takribani siku 21, wachezaji wametumika sana, hivyo katika mchezo wa leo (jana) ilikuwa ni nafasi kwa wachezaji wengine nao kutumika na wale waliotumika sana kupata mapumziko"
"Sio matokeo tuliyohitaji lakini mchezo huu umetupa manufaa kwa kuwapa nafasi wachezaji wengine kucheza. Umeona Shikhalo (Faruk) amecheza leo lakini kuna vijana tuliwapandisha kutoka Yanga B nao wamepata nafasi leo. Naamini kupitia mchezo huu kipo walichojifunza ambacho kitawasaidia huko mbele," alisema
Aidha katika mchezo huo Kaze alitumia mfumo wa 3-4-3, akimtumia kiungo Mukoko Tomombe eneo la ulinzi sambamba na Abdallah Shaibu na Said Juma