Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga wako visiwani Zanzibar ambapo leo majira ya saa mbili na robo usiku watashuka dimba la Amaan kuikabili Jamhuri Fc katika mchezo wa kombe la Mapinduzi
Wananchi walitua visiwani Zanzibar jana jioni kushiriki michuano hiyo ambayo hufanyika mwanzoni mwa kila mwaka kuadhimisha kumbukumbu ya Mapinduzi matukufu Zanzibar
Afisa habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema katika michuano ya mwaka huu, wamejipanga kuwa mabingwa hivyo mchezo wa leo wamedhamiria kuondoka na ushindi
Yanga ilitua Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili, ukiwaondoa Yassin Mustafa, Bakari Nondo, Feisal Salum, Deus Kaseke, Farid Mussa na Ditram nchimbi ambao wako na timu ya Taifa inayojiandaa na fainali za michuano ya CHAN zitakazofanyika baadae mwezi huu nchini Cameroon
Nahodha Lamine Moro nae atakosekana katika michuano hiyo akipewa ruhusa kurejea kwao Ghana kuiona familia yake
Huu ni wakati mwingine kwa mashabiki wa Yanga hasa kule visiwani Zanzibar kupata burudani kutoka kwa timu yao