Kumekuwa na tetesi nyingi kumuhusu mshambuliaji Mcongoman Idris Ilunga Mbombo anayeitumikia klabu ya Nkana Fc
Jina lake limetawala sana kurasa za Magazeti ya Michezo na mitandao ya kijamii ikielezwa amefanya mazungumzo na Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Usajili Injinia Hersi Said ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM
Gazeti la Mwanaspoti likafichua mshahara ambao nyota huyo ametaka alipwe na Yanga (Dola 10,000)
Kama Yanga itafanikiwa kumsajili mshambuliaji huyu, basi timu pinzani ziandike maumivu katika mbio za ubingwa
Mbombo (24) ni mchezaji mwenye urafiki na nyavu, akiwa katika kiwango bora sana wakati huu
Msimu wa 2018/19 akiwa na kikosi cha Nkana Fc, aliibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Zambia, akiweka kambani mabao 21
Katika msimu huo ambao alitimka Nkana na kujiunga na Al Hilal ya Sudan, Mbombo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu ya Zambia
Baada ya kuitumikia Al Hilal kwa muda mfupi, Mbombo alirejea tena Nkana ambapo msimu uliopita akaisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa ligi kuu ya Zambia
Mbombo akashika nafasi ya tatu katika orodha ya vinara wa mabao akiweka kambani mabao 14
Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu, Mbombo amejipambanua kwa kuwa mchezaji anayeweza kucheza peke yake mbele
Ni mchezaji mwenye mwili, nguvu na uwezo binafsi wa kuamua matokeo wakati wowote
Hivi karibuni uongozi wa Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Injinia Hersi Said, ulidokeza usajili wa mchezaji 'mkubwa' ambaye wanaweza kumnasa kabla dirisha dogo halijafungwa
Awali kulikuwa na uwezekano mdogo wa kumpata mchezaji huyo, lakini sasa wana uhakika watamshusha Jangwani
Mbombo mwenyewe amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti akisema kuwa anatamani kucheza na Tuisila Kisinda kwani anaamini akicheza na winga huyo, atafunga mabao mengi